Mambo yamebadilika, pumba mbalimbali ambazo kwa miaka mingi zimekuwa zikitupwa katika maeneo mengi ya Tanzania, sasa zimeanza kugeuka kwa kasi kuwa rasilimali muhimu inayochangia kupunguza matumizi ya mkaa unaotokana na miti.
Kwamba pumba sasa zimegeuka kama mojawapo ya bidhaa inayokuza ajira nchini, hii yote inatokana na ukuaji wa teknolojia ambayo sasa imesababisha baadhi ya Watanzania kuvumbua matumizi mbadala ya pumba ikiwamo kuyageuza kuwa mkaa wa kupikia.
Ezra Mahenge kutoka Mafinga ni kati ya Watanzania ambao wanatengeneza mkaa kwa kutumia pumba zinazotokana na mabaki ya mbao kwa kuanzisha kampuni ya familia waliyoipa jina la Mena Wood Briquetting Company Limited.
Mwaka 2018 Ezra Mahenge akiwa na kampuni yake hiyo ilishiriki mashindano ya Mkaa Mbadala yaliyoendeshwa na Shell Exploration and Production Tanzania kwa kushirikiana na ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) yaliyolenga kuhamasisha utunzaji mazingira nchini, ambapo waliibuka nafasi ya pili kwa kupata Sh200milioni pamoja na ushauri kutoka taasisi ya IMED; Institute of Management and Entrepreneurship Development.
Kampuni hiyo sasa inapanga kuimarisha shughuli zake ili kuzalisha kwa wingi zaidi mkaa pumba; inatamani kuwa namba moja kwa kuzalisha nishati hiyo nchini, huku dhamira yao kubwa ni kukuhakikisha wanawafikia Watanzania wengi zaidi.
Kwa sasa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ndio mteja mkubwa wa kampuni yao kwani inawasambazia asilimia 80 ya mkaa wote wanaotengeneza.
Wateja wengine ni Shule ya Panda hill, na kiwanda cha maziwa ChawaKim Dar er Salaam. Mahitaji ya soko kwa UDOM ni wastani wa boksi (pisi 16) 1500 kwa mwezi. Mahitaji ya kiwanda cha Chawakim ni boksi 280 kwa mwezi, na shule ya Panda Hill ni boksi 100 kwa mwezi.
Maeneo mengine ambayo yanatarajiwa kusambaziwa mkaa ni Hospitali ya Mirembe, Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Kambi ya jeshi Makutupola, Kambi ya Jeshi Ihumwa na Shule za sekondari za bweni tano.
Kampuni hiyo imejipanga kutafuta masoko zaidi katika maeneo mbalimbali nchini lengo likiwa ni kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanajikita mizizi katika matumizi ya mkaa mbadala kwa mategemeo kwamba yatasaidia kupunguza matumizi ya mkaa unaotengenezwa kwa kutumia miti, kwani zaidi hutokana na kutaka miti katika maeneo mbalimbali hivyo kuharibu mazingira.
Uwepo wa kampuni ya Mena utasaidia kutoa huduma za nishati mbadala, ambazo ni salama, na zenye gharama nafuu ambazo zinajali hali ya uchumi ya jamii kwa ujumla. Pia, biashara hii itazalisha fursa nyingi za ajira kwa jamii inayozunguka.